Wednesday, June 8, 2011

WAKENYA WATUFUNIKA!! SIYO MBAYA!

Eti jamaa yangu mmoja alinishangaa kwa kunywa maziwa ya Brookside dairy, yatokayo Kenya. Eti nipendelee viwanda vya nyumbani, hivyo ninywe Tanga Fresh. Nyumbani wapi? Nani kasema utakapo ni Tanzania? Ni ushamba huo.

ebu fikiria mimi muhaya ningekuwa nakula matoke tu, hapa Dar Es Salaam, je, mlima mpunga angepata wapi soko? ebu fikiria ningeamua kula samaki wa ziwa victoria tu,maharage ya Mbeya angenunua nani?

Na nani aliyetudanganya na hii dhana ya mipaka ya nchi? Miaka 200 iliyopita hatukuwa na Kenya, Uganda, wala Tanzania kama tunavyoziona hizi nchi sasa. Leo hii naambiwa ninywe maziwa ya Tanga fresh, kwanini?

Ni mtu huyo huyo ananiyeshangaa mimi kunywa maziwa ya Brookside, anaye shabikia Machester United na kushindwa kutaja 'line up' ya Simba, vijana wa Msimbazi.

Hii ni Dunia ya utandawazi, ambayo mwandishi Thomas Friedman, anaiita 'Flat World'.Mimi kama mteja natakiwa ninunue kitu roho yangu inapenda bila kipingamizi chochote. Hiyo ndiyo faida ya utandawazi.

Na nchi zilizokumbatia utandawazi zimefanikiwa sana. Angalia Marekani, ambapo vipaji kutoka India ( software), africa ( sanaa),China ( bidhaa zote) nk vinaiweka Marekani hapo ilipo sasa.

Hii ni dunia ya wingi, ( abundance) na hatutaweza kuishi hapa Duniani kama tutakuwa ni viumbe tunaotaka kujifungia na raslimali zetu tulizonazo. Kama kuna ardhi tugawe tu, kama kuna ajira tugawe tu, kama kuna walaji tuwaruhusu wananunue bidhaa za nje bila kipingamizi.

Serikali inachoweza kufanya ni ubunifu, na umakini wa kunufaika kutokana na bidhaa, ujuzi( skills) na mitaji kutoka nje. Serikali iliyo makini itatoza kodi na kutoendekeza misamaha ya kodi kwa wageni wanaokuja nchini kwetu.Serikali iliyo makini itaendelea kutoa motisha kwa viwanda vya maziwa vya hapa nchini ili vishindane na Brookside kutoka Kenya. Je kuna ubaya gani kwa kabaila kutoka Kenya akichukua ardhi na kulima halafu akapewa masharti kuwa mazao asilimia kubwa auze Tanzania? Si bora kuliko kukaa na mapori yasiyolimwa?

Tafakari, Chukua hatua.

1 comment: