Saturday, November 19, 2011

UCHUMI WA KAGERA WAWEZA KUFUFULIWA

MKOA wa Kagera ulikuwa ukiitwa mkoa wa Ziwa Magharibi (West Lake). Ulipata jina la sasa mwaka 1979, baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda.

Hivi vilikuwa vita vya kumfukuza na hatimaye kumwondoa dikteta Iddi Amin wa Uganda aliyekuwa amevamia Tanzania.

Amin alivamia na kukalia eneo la Kagera akidai kuwa mpaka halali kati ya nchi hizi mbili ulikuwa Mto Kagera; pale Kyaka.

Kwa wenyeji wa mkoa huu, neno Kagera linatokana na “Akagera,” yaani kijito kinachotiririsha maji yake katika mto mkubwa au ziwa. Mto Kagera hutiririsha maji yake katika Ziwa Viktoria.

Maji haya ya Kagera huonekana wazi kuwa hayakai ziwani bali hukatisha ziwa na kuwa chanzo cha Mto Nile ambao ni mto mrefu kuliko yote duniani.

Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa michache iliyobahatika kupata maendeleo makubwa kiuchumi na kijamii kabla na baada ya uhuru.

Wamisionari wa madhehebu ya Kilutheri na Wakatoliki (Missionaries of Africa/White Fathers), waliingia Bukoba mwishoni mwa miaka ya 1880 na kuanzisha shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.

Moja ya vyuo hivyo ni Chuo cha Ualimu cha Kajunguti, katika wilaya ya Muleba. Chuo hicho kilikwishafungwa. Miongoni mwa shule za sekondari zilizoanzishwa na wamisionari ni St. Thomas More College (Ihungo) na Nyakato.

Wamisionari pia walifungua hospitali mbalimbali na vituo vya afya. Miongoni mwa hospitali hizo ni Rubya, Kagondo na Ndolage, zote za wilaya ya Muleba; Mugana (Misenyi), Biharamulo, Nyakahanga na Isingiro, wilayani Karagwe na Murugwanza, wilayani Ngara.

Kwa takriban miaka 500 sasa, wakazi wa mkoa wa Kagera wamekuwa wakistawisha migomba kwa ajili ya chakula (ndizi) na mibuni – kwa ajili ya biashara (kahawa).

Wakulima wa kahawa walianzisha ushirika wao chini ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Bukoba Cooperative Union (BCU), ambacho kilianzishwa mwaka 1948.

Miongoni mwa waanzilsihi wa BCU ni mzee George Clement Kahama, ambaye alishika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Kupitia ushirika wao, wakulima wa Kagera waliweza kusomesha watoto wao ndani na nje ya nchi. BCU iligharamia masomo ya wanafunzi hao.

Wakulima pia walianzisha umoja wa aina ya sasa ya Kuweka na Kukopa, maarufu kama “Ihanika.” Hadi miaka ya 1955, mfuko huo ulikuwa na zaidi ya Sh. 400 milioni.

Lakini uchumi wa mkoa na wananchi ulianza kuonyesha mdororo baada ya uhuru. Inaonekana kuwa nguzo kuu zake zilianza kulegea na hatimaye kung’oka.

Utawala wa asili wa kichifu ulitupiliwa mbali. Pamoja na mfumo huo kuwa wa upendeleo kwa watawala na hata kuhalalisha unyonyaji kwa njia ya miliki ya ardhi, ulikuwa na taratibu shinikizi zilizowezesha uwajibikaji kimila na hasa katika uzalishaji mashambani.

Hili lilifuatiwa na mpango wa serikali wa kuweka ushirika chini yake badala ya kuwa mikononi mwa wananchi.

Katika mazingira haya, hata mfuko wa wananchi, Ihanika, ukatoweka na serikali haikufanya juhudi kuwafidia. Hapa uchumi uliokuwa umeshamiri ukaingia misukosuko.

Kwa miaka mingi, wananchi wa Kagera walikuwa wakifanya biashara na wenzao wa Uganda. Utawala wa Amin uliondoa ushirikiano na kupunguza mwingiliano.

Kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 kulikofuatia, kuliziba vifereji vya mahusiano ya kiuchumi yasiyorasmi vilivyokuwa vimesalia.

Vita vya Kagera (1978/79), vilipiganiwa katika ardhi ya mkoa wa Kagera. Biashara ndogo na kubwa ziliharibika. Mtindo wa maisha ulivuruguka. Wananchi wakawa wakimbizi ndani ya nchi yao. Uchumi ukaanguka zaidi na umasikini ukashamiri.

Watu wengi walifariki katika vita. Mali zao ziliharibiwa pamoja na miundombuinu – barabara, shule, hospitali na mabenki.

Rais Julius Nyerere alitoa miezi 18 kumaliza matatizo hayo na kurejesha maisha katika hali ya kawaida; lakini miezi hiyo haijaisha hadi leo.

Ndipo ikaja “Operation Uhujumu Uchumi” mwaka 1983. Zoezi hilo liliendeshwa chini ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali Nsa Kaisi.

Katika sakasaka na kamatakamata, watu wengi waliswekwa ndani; mali zilikamatwa, baadhi walifilisiwa kwa halali au haramu na, katika hali isiyo na maelezo, baadhi ya mali, zikiwa zimeharibika, zilirejeshwa kwa wenyewe bila hata “pole.”

Kukamatwa kwa magari (malori), kwa mfano, kulisababisha maisha magumu vijijini kwa kuwa wananchi hawakupata mahitaji.

Wakati huo, vyama vya ushirika ambavyo sasa vilikuwa vimerejeshwa chini ya mfumo wa kiserikali, vikawa vimeingiliwa na kile wanaita “mchwa.”

Watu wasiokuwa waaminifu wakajipenyeza na kuwaibia wakulima wa kahawa. Imani ya wananchi ikapungua. Ari ya kilimo ikaanza kupotea.

Hapa ushirika wa BCU/KCU uliokuwa na nguvu, ukameguka. Wananchi wa wilaya ya Karagwe wakajitenga na kuanzisha Karagwe District Cooperative Union (KDCU). Biharamulo nao wakajitenga wakaanzisha Biharamulo Cooperative Union (BCU).

Yote haya yalikuwa na athari mbaya kwa uchumi na maisha ya wananchi mkoani Kagera.

Kana kwamba hayo yalikuwa hayatoshi, ukaingia ugonjwa wa ukimwi. Mgonjwa wa kwanza wa ukimwi aligundulika mkoani Kagera mwaka 1983.

Uzito wa janga hilo unashuhudiwa kwa makaburi “mabichi” yaliyojaa mashambani. Vijana waliokuwa wakichakarika kwa kufanya biashara, wamekufa kwa kasi isiyomithilika.

Wakati mwingine waweza kutembelea nyumba moja na kukuta pikipiki tatu au nne zimeegeshwa. Ni za vijana waliokufa “kwa ukimwi” ambao walikuwa watafutaji wa neema kwa familia.

Hivyo wazalishaji wakubwa wakaangamia kwa ukimwi. Wakabaki wazee. Familia nyingi zikawa na mzigo wa kutunza yatima. Muda mwingi wa kuzalisha mali ukapotea kuuguza wagonjwa, kutunza yatima na kuhudhuria mazishi na matanga.

Ndipo likaja janga la kuzama kwa meli – mv BUKOBA, tarehe 21 Mei 1996. Inakadiriwa wengi wa abiria waliokufa katika ajali hiyo walikuwa wa mkoa wa Kagera; wengi wao wakiwa vijana watafutaji waliokuza uchumi wa mkoa.

Sasa kumezuka ugonjwa wa kunyausha migomba (Banana Xanthomonas Wilt-BXW) na ugonjwa wa kahawa (Coffee Fusarium Wilt-CFW).

Kama hakuna kahawa na hakuna migomba (ndizi), siyo tu uchumi bali maisha ya wananchi yako hatarini. Hakujawa na mbadala wa maana.

Nani ataisemea Kagera? Kuna matatizo mengi lakini mengine yaweza kuwekwa kwenye ngazi ya changamoto.

Je, tukianza na kongamano kubwa la wanaoitakia mema Kagera, hatuwezi kutotoa njia za kuinua uchumi na maisha ya wananchi mkoani?

Mkoa una hali ya joto la wastani la sentigredi 26.02. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800 hadi 1,200 kwa mwaka – kati ya Septemba na Januari na kati ya Machi na Mei.

Inawezekana.

Makala hii ilitokea kwenye gazeti la MwanaHalisi la tarehe 25/MAY 2011

1 comment:

  1. basi hizo million 400 nyerere alizichukua na ndio ulikuwa mwisho wa maendeleo ya mkoa wetu hata chuo cha ualimu kajungute ndiye alikiua kwa kisingizio kuwa kagera tumeishaenderea,ndio maana nikifika hapo ninakuwa na hasira naye yaani simpendi

    ReplyDelete