Nyegera waitu Bukoba mjini!
Padri Privatus Karugendo Machi 3, 2010
LEO napenda kuzungumzia mji wa Bukoba ambao ndiyo makao makuu ya Mkoa wa Kagera. Kuna njia kuu tatu za kuingia mji wa Bukoba. Unaweza kuingia kwa barabara, kwa ndege au kwa meli.
Ukiingia Bukoba kwa ndege utatua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba ulio ufukweni mwa Ziwa Victoria ambao kwa sasa unafanyiwa ukarabati mkubwa wa upanuzi. Ukiwa unakaribia kutua unaweza kuwa na mawazo kwamba labda utatua majini au kwenye kisiwa cha Musira kilicho karibu sana na mji wa Bukoba.
Uwanja huu umelikaribia sana ziwa kiasi cha kuleta woga wakati ndege inatua na kupaa. Ingawa uwanja huu unaonyesha dalili za kutisha wakati wa kutua, si ajali nyingi zimetokea. Kumbukumbu zinaonyesha ndege mbili za jeshi kupata ajali katika uwanja wa Bukoba.
Ajali ya kwanza ilitokea wakati wa vita ya Kagera. Ndege ya jeshi ilikuwa inaruka ikakosea mwelekeo na kukiparamia kisiwa cha Musira. Miaka ya karibuni ndege nyingine ya jeshi ilikosa mwelekeo wakati ikitua na kuziparamia nyumba za wenyeji.
Ndege nyingine ya Precision Air iliokolewa na matuta; vinginevyo ingeserereka hadi ziwani. Jambo la msingi ni kuomba usiku na mchana isitokee ajali nyingine hadi uwanja huu utakapopanuliwa.
“Nyegera waitu”; ikimaanisha: Karibu Bwana ni neno la kwanza utakalolisikia Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Baada ya neno hilo, ni mfululizo wa mchanganyiko wa Kihaya na Kiingereza. Mfano: “Omundege twaija comfortably bwana” – ikiwa na maana kwamba safari ya ndege ilikuwa shwari.
Nyegera waitu unaisikia pia ukiingia Bukoba kwa njia ya meli. Bandarini, wenyewe wanaita Kastamu, Nyegera zinakuwa nyingi sana; maana watu wengi wanasafiri kwa meli zaidi ya ndege.
Neno jingine utakalolisikia ni Waiyukayo; ikimaanisha pole ya safari. Neno hili halikusikika sana siku za nyuma. Limeanza kusikika mwaka 1996 baada ya ajali ya MV Bukoba.
Watu zamani walikuwa na imani na usafiri wa meli. Waliamini meli haiwezi kupatwa na ajali. Siku hizi kila anayepanda meli na jamaa zake wanaobaki nyuma wanakuwa na wasiwasi.
Safari hii ya meli ni ya usiku. Meli ya Victoria inachukua muda wa saa nane hivi kutoka Mwanza hadi Bukoba. Meli ndogo kama vile Serengeti inachukua karibu saa 12 kufika Bukoba. Marehemu Kalikawe aliimba wimbo kwamba meli ni kama Nyumba kubwa. Watu wanakula, wanakunywa na kulala….wakati mwingine mtu anaomba Mungu, na kufumba macho ili asiyaone yale yanayotendeka melini!
Siku MV Victoria ilipopoteza mwelekeo na kuingia nchi kavu, watu waliamini kuna kitu kilikuwa kinaendelea kwenye vyumba vya makapteni. Walinogewa hadi asubuhi na kusahau usukani!
Kuna barabara kuu mbili zinazoingia Bukoba mjini. Inategemea unaingia kutokea wapi. Kuna barabara ya Mwanza na Barabara ya Uganda. Zote mbili zinaungana kuwa barabara moja Kilometa moja kabla ya kuingia Bukoba mjini.
Kwenye kituo cha mabasi utaisikia tena Nyegera waitu na Waiyukayo ambayo inamaanisha Pole ya safari. Na inakuwa kweli na maana hiyo pole ya safari; kwani ukifika Bukoba mjini bila basi lenu kutekwa na majambazi ni lazima kumshukuru Mwenyezi Mungu!
Serikali imeshindwa kabisa kuwakamata majambazi hao. Kuna mchezo hapa wa nani amvike paka kengele. Wananchi wanawajua majambazi na wakati mwingine serikali inawajua majambazi.
Ni mpaka pawepo na uwazi na nia kwa pande zote mbili ndio tatizo hili litakwisha. Vinginevyo ningekushauri usitembelee Bukoba wakati wa kipindi cha Krismasi!
Mji wa Bukoba umezungukwa na vilima. Kuna Kilima cha Ihungo. Hapo kuna Sekondari ya zamani iliyokuwa ikujulikana kwa jina la St Thomas Mores College. Wasomi wengi nchini wamepitia kwenye shule hiyo.
Kilima kingine ni cha Kashura. Kilima hiki kinakaliwa kwa wingi na ELCT. Wamisionari walijenga hapo. Ni sehemu nzuri inayokufanya ulione ziwa Victoria vizuri na kuuangalia vizuri mji wa Bukoba.
Hata hivyo, Bukoba inaonekana vizuri zaidi ukiwa kwenye kilima cha Kishasha. Kilima hiki kina majumba mazuri ya kisasa ambayo kwa wale wasio na uwezo wa kuona mbali ya pua zao, wanayaita takataka na uchafuzi wa mji!
Ukiwa hapa unaweza kuona tatu ya nne ya mji wa Bukoba. Unapata picha nzuri ya Bukoba; jinsi mji ulivyozungukwa na milima na kuwa ufukweni mwa ziwa Victoria.
Pamoja na yote unayoyasikia kuhusu Bukoba utashangaa sana kuona maisha yanaendelea kama kawaida. Hakuna anayeogopa UKIMWI. Ukitaka kukutana na mwanamke au msichana na ukiamua kutumia KONDOMU au kutotumia, mwanamke atakwambia uamuzi ni wako.
Maana yake ni kwamba unaweza ukatumia kama unapenda au usitumie. Vituko vya nani kafumaniwa na nani ni vingi mno mjini Bukoba kuzidi kipindi kile kabla ya ugonjwa huu wa hatari haujapiga hodi.
Kama unayapenda maisha yako, ni lazima uingie Bukoba kwa uangalifu mkubwa sana. Mji unaonekana kuwa mzuri sana. Watu ni wakarimu kweli. Nyegera ni nyingi, lakini usipoangalia unaweza kupata Nyegera ya moja kwa moja!
Habari za mitaani ni kwamba kuna watu wenye pesa ambao ni waathirika wa UKIMWI. Watu hao wamepania kueneza ugonjwa huo. Wanatumia pesa zao kusambaza ugonjwa huo. Wanahakikisha wametembea na wanawake, wasichana wadogo kwa wakubwa. Wanatumia pesa zao kuangamiza kizazi kizima.
Watu hawa wana uwezo wa kununua dawa za kusogeza mbele maisha (ARVs); wana uwezo wa kula vizuri na kutunza afya zao. Wana uhakika wa kuishi maisha marefu kidogo. Hawajali kama watu wanaowaambukiza virusi wana uwezo kama wao.
Hivi ni kati ya vituko vya kusikitisha utakavyokumbana navyo mjini Bukoba. Kila mtu anajua juu ya jambo hili. Viongozi wa serikali wanalijua hili na viongozi wa dini wanalijua. Hakuna mtu wa kuwakanya; maana hawa ni watu ‘muhimu’ sana kwa serikali na kwa dini. Ni watu wanaotoa michango mizito serikalini na kwenye madhehebu mbalimbali.
Huwezi kutembelea Bukoba na usikose kuingia kwenye soko la Bukoba mjini. Vyakula utakavyoviona ni kama vile unavyoweza kukuta kwenye masoko yote ya Tanzania. Labda tu kwamba ndizi zitakuwa ni nyingi kupita sehemu nyingine unayoijua.
Mbali na ndizi, kama ni mwezi wa Novemba Au Aprili, utakuta senene. Senene ni aina ya wadudu wanaopendwa na Wahaya. Ni chakula cha heshima. Binti anayechumbiwa ni lazima kupeleka zawadi ya senene kwa mchumba wake.
Mwenye nyumba, baba wa familia, akiwa safari ndefu – tuseme safari ya kumchukua miaka mitatu, ni lazima mama wa nyumba atunze senene za kila mwaka. Atafunga mafungu mafungu hadi bwana atakaporudi.
Bibi mwenye wajukuu, ni lazima afunge mafungu ya senene kwa kila mjukuu. Wajukuu wanapomtembelea kila mjukuu anapata fungu lake! Mtu ukipewa senene ni lazima kuna kusema asante. Mara nyingi asante hii inakuwa ni kitenge, kanga au pesa.
Zamani senene walikamatwa mbugani. Lakini siku hizi wataalamu wamegundua namna ya kuwakamata kwa urahisi. Wanatumia taa za umeme zenye mwanga mkali. Taa hizi zina uwezo wa kuwavuta senene kutoka sehemu za mbali hadi Kilomita kumi.
Wakati wa msimu wa senene wataalamu wa Bukoba mjini wanaweka taa za umeme zenye mwanga mkali kwenye paa za nyumba ili kuwavuta senene. Hii ni biashara nzuri; maana mtu mwenye taa ya mwanga mkali anawatoza pesa watu wanaofika kwake kukamata senene! Zoezi hili ni la kila mwaka hasa mwezi wa Novemba na Machi.
Wahaya wanalima kahawa. Hili ni zao kuu la biashara. Jambo la kushangaza ni kwamba pamoja na kulima kahawa, watu hawa hawanywi kahawa! Hata wale wachache wanaokunywa kahawa, watakwambia wanakunywa Chai (ka-chai).
Wakati bei ya kahawa inaendelea kushuka kwenye soko la dunia na kuathiri kiasi kikubwa uchumi wa mkoa wa Kagera, inashangaza sana Wahaya kulalamikia bei mbaya ya kahawa wakati wao hawanywi kahawa yao! Badala ya kunywa kahawa wana utamaduni wa kutafuna kahawa, na hii ni ishara ya upendo.
Ukimtembelea mtu nyumbani kwake, asipokukaribisha kwa kahawa za kutafuna, ni ishara ya kutokuwepo na upendo kati yenu. Hata hivyo, kiasi kinachotafunwa ni kidogo sana kiasi cha kuweza kupandisha bei ya kahawa.
Kuna haja ya Wahaya na Watanzania kwa ujumla kujenga tabia ya kunywa kahawa kwa lengo la kulinda soko na bei ya kahawa.
Wahaya wanapenda dini. Hili utalitambua kwa misikiti mikubwa na makanisa yaliyo mjini Bukoba. Ukisimama kwenye kilima chochote kile kinachouinamia mji wa Bukoba, utaona misikiti na makanisa ikichomoza.
Utauona msikiti wa Uswahilini uliojengwa kwa mtindo wa kisasa. Utaliona Kanisa Kuu la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) ambalo linajulikana kama kengele tatu. Linaonekana kuupamba mji wa Bukoba na kuonyesha kwamba mji huu ni wa wacha Mungu.
Nayo Cathedral ya Wakatoliki inafanyiwa ukarabati. Sasa hivi ni zaidi ya miaka kumi tangia ukarabati huo uanze. Ni kanisa kubwa na la kuvutia. Mnara wake unaonekana ukichomoza kuyazidi majengo yote ya Bukoba mjini na kutangaza utukufu wa Roma.
Kanisa hili ndio litakuwa kaburi la marehemu Kadinali Rugambwa. Sasa hivi amezikwa kwenye kaburi la muda kwenye Kanisa la Kashozi. Kwa nini ukarabati wa kanisa hili umechukua muda mrefu? Kila mtu anajua jibu! Lakini kila mtu anafunga mdomo wake! Wale wanaothubutu kusema wanatumia mafumbo.
Lugha ya Kihaya inatumia mafumbo mengi. Ni lazima ujifunze lugha ya mafumbo ukiwa Bukoba. Ukisikia maji usifikiri ni yale ya kunywa na ukisikia chakula usikimbilie meza ya chakula. Hata kituo kipya cha redio kilichoanzishwa mjini Bukoba kijulikanacho kama Kasibante, ni mafumbo matupu. Maana yake inaelekea ni “kumfunga ng’ombe”. Kwa historia ya kiti cha ubunge cha Bukoba Mjini, na ikizingatiwa mmiliki wa Redio Kasibante, ujumbe wa fumbo uko wazi!
Kanisa la Orthodox limeingia kwa nguvu mjini Bukoba. Kanisa lao linapamba kilima kimojawapo kinachouinamia mji wa Bukoba. Pia wamejenga kanisa zuri mjini Bukoba na wanaendelea kujenga makanisa mengine vijijini.
Usishangae kukutana na watoto wengi wa mitaani mjini Bukoba. Pamoja na kwamba watu ni wacha Mungu, wana makanisa mazuri na misikiti mizuri (na kusema kweli makanisa na misikiti inajaa waumini), hakuna anayewajali watoto wa mitaani.
Ukizungumza na watoto hao kwa karibu, utashangaa sana kujua kwamba watoto wengine baba zao ni viongozi katika makanisa na misikiti. Ndio hivyo! Jinsi wanavyosali sana na kumcha Mwenyezi Mungu, ndivyo pia na madhambi kibao.
Mengine sitaki kuzungumza. Acha ukutane nayo mwenyewe. Acha uambiwe Nyegera waitu. Kama wewe ni mtu wa familia, chunga sana usijenge nyumba ndogo Bukoba. Kama wewe ni kijana ambaye hujapata jiko huwezi kukwepa kuitwa Omwami wange (Bwana yangu).
Wengi waliopitia mjini Bukoba wakati wa ujana wao wameoa Bukoba au wana ‘nyumba ndogo’. Sitopenda kuwataja!
Bukoba ni mahali pazuri kweli. Kama wenyewe wanavyoisifia. Pana Ziwa Victoria, pana mito mizuri inayotiririka na kuifanya Bukoba ionekane kijani wakati wote. Ina mvua mwaka mzima. Kama si uvivu wa Wahaya, wangeweza kulima na kuilisha chakula Tanzania nzima.
Bukoba ina vilima na mabonde; vitu vinavyoipamba na kuipendezesha. Bukoba ina vivutio vingi vya kitalii. Bukoba ni nzuri! Hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro. Kasoro hizo nimezitaja moja baada ya nyingine. Kama unataka nizirudie nitakwambia Nyegera waitu.
_________________
The longest journey starts with the first step - Chinese
If you do not stand for something, you will fall for anything. - Unknown
florianrobert
please visit www.mtukwao-florian-florian.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment