Friday, May 6, 2011

IKO WAPI BANDARI YA SALAMA??

Hivi hapa Dar mimi naona wote tunapoteza muda na suit zetu na jeans zetu kusaka pesa mtaani. Tumegeuka wachuuzi wa bidhaa kutoka nje, takribani China na ughaibuni. Angalia biashara zetu zote, makampuni ya bima, viwanda uchwara tulivyonavyo ambavyo vingi vinapokea malighafi kutoka viwanda vingine vya nje ya nchi hivyo kuzidisha ufinyu wa pesa zetu za kigeni,makampuni ya kichuuzi kama Sigara, kampuni za simu ambazo nazo zipo hapa kuvineemesha viwanda vya simu vya China na Ulaya. Kwa mwendo huu hatufiki popote.


Ebu fikiria, Dar tuna bandari ya asili ( natural harbour) ambayo Mungu hatutozi kodi hata senti moja. Holland inategemea sana Roterdam kama kitego uchumi chake cha maana. ( Roterdam) ni bandari kama ilivyo Dar Es Salaam. Wateja tunao wengi ambao wanatakiwa wailetee bandari yetu pesa nyingi za kigeni. Zipo nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Congo, na Zambia ambazo hazina bahari hivyo kutegemea sana bandari ya Dar Es Salaam kama geti la kuchukua na kupeleka mizigo yao nje ya nchi. Lakini cha ajabu Bandari ya Dar imebanwa na majengo mengi ikiwemo Ikulu yasiyoleta tija kwa nchi. Kwanini tusibomoe majengo yasiyofaa na kuongeza gati pale magogoni hivyo kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar kama kitego uchumi cha nchi.

Mwalimu Nyerere alikuwa Kiongozi mwenye maono ( vision). Yeye aliamua kuhamisha makao makuu ya Serikali kuelekea mji uliopo katikati ya Tanzania, yaani Dodoma. Kimkakati ( strategically) alikuwa sahihi, kwani Dodoma ni kati kati ya nchi. Lakini katika makosa ya kiuchumi aliyoyafanya Nyerere, kwa hili alikuwa sahihi kwa asilimia 100%. Dar ungebaki kuwa mji mkuu wa kibiashara na Dodoma makao makuu ya Serikali. Kwa vyovyote vile maji ufuata mkondo na siye wengine tungeifuata serikali Dodoma na maofisi yake.

Haya ni mawazo yangu.

No comments:

Post a Comment