Wednesday, May 4, 2011

UGUMU WA MAISHA WAKIMBIZA UCHUNGU WA KUJIFUNZA

Tunaelekea wapi waafrika/watanzania??? nafikiri ugumu wa maisha unapoteza nia nzima ya kujifunza ( learning process); Enzi hizo kabla ya kuja kwa wakoloni, ilikuwa ni kawaida kwa mzazi kupoteza muda wa kutosha na mtoto wake akimfundisha maisha. Muhunzi alimfundisha mtoto wake uhunzi, mvuvi alienda na mwanae kuvua samaki,mchonga vinyago alimfundisha mwanae ujuzi wa kutosha kuhusu shughuli yake. Matokeo yake ujuzi uliridhishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Ushaidi wa haya upo, leo tujiulize kwanini wamakonde ni wajuzi wa kuchonga vinyago, na kwanini wamasai ni wataalam wa kutengeneza nguo zako za kimasai zenye rangi ya kuvutia? Umahili huo wa makabila yetu una mvuto mkubwa hasa kwa wageni pale wazungu wanapotoa dola zao kununua kazi zetu za asili. 'Our precious work of art'

Ujio wa mkoloni ulififisha utu wa mwafrika na yeye ( mwafrika) kujiona dhaifu mbele ya mzungu.( inferiority complex); Wazungu waliizita jadi/utamaduni/ na uchumi wetu wa kishenzi ili tu wapenyeze utamaduni na uchumi wao. Wazungu hao wakaanzisha uchumi wa pesa ( money economy) na kumfanya kila mwafrika aangaike kuitafuta pesa ili kulipa kodi ya kichwa tuliyolazimishwa kwa mtutu wa bunduki tuilipe. Ili kuilipa kodi ya kichwa ilibidi masikini wazee wetu wauze ujira wao mashambani wakilima pamba,kahawa,karanga,miwa, yote ikiwa ni kwa ajili ya soko la ulaya. Kibaya zaidi wazee hao hao wakaletewa mabaki ya kutoka ulaya na wakatumia pesa hiyo hiyo waliyoipata kulimia pamba ili kununulia nguo kukuu zilizokuja kutoka ulaya.

Huo ndio ukawa mwanzo wa kifo cha kutaka kujifunza, Wahunzi wakatundika darini vifaa vyao vya uhunzi,wafua chuma wakatupilia mbali vifaa vyao, wavuvi wakaacha uvuvi ili walime pamba ambayo mzungu alichagua ndilo zao la kununua. Mtoto akaanza kuachwa kufundishwa na Baba yake, saratani hiyo imetushika mpaka tarehe ya leo.

Lakini aliyetangulia katika mfumo fulani ametangulia tu, na hauwezi kumshika. Waingereza tayari walishazindua mapinduzi ya viwanda ( industrial revolution) kati ya 1750-1850. Hawa waliweza kuzalisha kwa wingi na ziada kiasi kwamba mabaki au makapi ya bidhaa zao ziliingia kwa wingi Afrika. Kama tunamuona mchina anajaza bidhaa Afrika leo, basi Muingereza alianza zamani tangu enzi za mababu zetu.

Wazungu hao wametupangia tuzalishe bidhaa fulani tu, tena zile zinazotokana na kilimo, ambacho kilinyimwa ubunifu wa kutosha hivyo kutoa mazao machache na duni. Matokeo yake mazao yetu yamekuwa yakituletea tija hafifu sana hisiyoweza kukidhi mahitaji yetu yaliyopandikizwa, ( artificial)

Kila kukicha, mzazi anaikimbiza shillingi, ingawa hakuna hata siku moja haitamtosha kwani anazalisha bidhaa duni hisiyoweza kukubalika kwenye soko la dunia.Mwafrika huyu anapoteza muda mwingi kulima eka moja na kutoa mazao hafifu mno na hivyo kukosa muda wa kumfundisha mtoto wake ujuzi wa shughuli anayoifanya.

Angalia kwenye miji yetu, hakuna viwanda, sisi wote ni wachuuzi. Watoto wetu wanakwenda shule yenye mtaala wa kizungu huku wakipata elimu duni ambayo haitawawezesha kuingia soko la kazi la dunia ( world labour market) kikamilifu kama wenzao wa Japan. Sababu ya mtoto wangu anayesoma shule ya kutwa kushindwa kuingia kwenye soko la kazi la dunia ni kwa sababu soko hilo siyo la kwake kiasilia. Kosa lilifanyika pale babu yake aliponyimwa fursa ya kuendeleza uhunzi na kujiunga na soko lililotangulia mbele mno kupita kiasi.

TUTABAKI TUNAFUKUZA UPEPO WA TEKNOLOGIA BILA KUWAKAMATA WAMAGHARIBI

jamani tuwe waafrika.

No comments:

Post a Comment