Thursday, June 2, 2011

TUKIWEKEZA KWENYE KUPENDANA,MATATIZO YOTE YATAISHA

Sipendi waafrika tunavyoyachukulia matatizo yetu, inaonekana hata wanasiasa wanachukulia matatizo kama mtaji wa kisiasa, na hata wafanyabiashara wanachukulia matatizo kama mtaji wa kujijazia mali.Wasomi nao wanachukulia matatizo kama mwanya wa kujikimu na kujilimbikizia mali. Haya yote yangeonekana kuwa historia kama tungewekeza wote kama waafrika kati jambo moja muhimu. Kupendana, au kwa kiingereza LOVE.

Kwanini tuna Ukimwi? kwanini watoto wetu hawajui kusoma na kuandika? kwanini ugonjwa wa malaria tunashindwa kuutokomeza?

Jibu ni moja, HATUPENDANI!!! Matatizo yetu yanatokana na siye wenyewe kushindwa kugawana kwa haki bin haki mali zetu ( resources) na hivyo kupelekea kukaribisha mabalaha kibao. Rhonda Byne katika kitabu chake 'Secrets' anaandika kuwa kila ugonjwa unaanza na mawazo potofu,( negative thoughts).Mchukulie Mzazi mzembe anayetoka kazini saa tisa mchana na kuelekea baa mpaka saa nane usiku; mzembe huyu anafika nyumbani wakati mke wake na watoto wameshalala. Tujiulize, ana upendo huyu kwa familia yake? Je, watoto wake wakikosa muongozo wa Baba na kuishia kuwa watoto wa mitaani ni nani wa kulaumiwa? Je tutegemee watoto waliolelewa na Baba mwenye mawazo hasi wataibuka kuwa viongozi wa kesho wenye mawazo chanya?

Sisi wazazi hata kama tukichoma pesa zetu zote kupeleka watoto kwenye shule zenye ada ya vyuo vikuu, bila ya kuwa na ukaribu na watoto wetu tunakaribisha jamii duni hisiyokuwa na mwelekeo imara. Tunatengeneza wezi wa dot.com,( matapeli wa kimataifa walioenda shule), tunatengeneza wala rushwa, tunatengeneza wavuta bangi na madawa ya kulevya, na tunatengeneza kizazi kisichokuwa na maadili.

Watoto kupata elimu bora ni jambo moja, lakini watoto kuwa na maadili ni jambo lingine ambalo naona linapotea kila kukicha. Leo hii upendo, uaminifu na uungwana unapotea kwa kasi kubwa. Hata makanisani na misikitini kila mtu anakula kwenye dawati lake.Nani atamfunga paka kengele?

Kwa mwendo huu tunafikiri UKIMWI tutautokomeza wakati waganga wataalam wakubwa tuliowasomesha kwa taabu wanaacha kutibia malaria na kukimbilia kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofadhiliwa na watu wa Marekani? je, utawalaumu wakati tangia watoto hawakufundishwa kupendana na wazazi wao? Kwani hatufahamu kuwa kinga zetu zinafifia sana mgonjwa wa malaria anaposhindwa kutibiwa? Je inaingia akilini tunaposhindwa kusisitiza usafi wa kawaida kabisa na kupeleka nguvu kwenye gonjwa la ukimwi?

Tafakari, Chukua hatua.

No comments:

Post a Comment