Tuesday, November 3, 2009

MIAKA 40 YA MTANDAO;HAPA AFRIKA NGOMA YA KIZUNGU YACHEZEKA KWA TAABU!


Afrika ina makabila mengi yenye tofauti kubwa ya kimtazamo, kimila na desturi. Hata tunapocheza ngoma wandebere wa Afrika kusini uchezaji wake ni tofauti na wagogo wa Dodoma, Tanzania.Kila kabila ina mila na desturi zake zilizotokana na historia na mapokeo ya kabila husika. Ni vigumu sana kwa mpemba kucheza ngoma ya kimasai na hii inatokana na sababu nyingi za kihistoria, kistaarabu na mapokeo ya makabila hayo mawili ambayo yanatofautiana sana. Wamasai hucheza kwa kurukaruka juu huku mashuka yao yakiachia wazi sehemu zao za utupu. Wapemba ambao wanamapokeo ya ustaarabu wa kiislamu kuonyesha utupu wao ni kinyume cha dini yao.

Miaka 40 iliyopita, (1969) saa tatu usiku ya tarehe 29th October, wahandisi wa kimarekani waliochanishwa kwa umbali wa miles 400 kati ya Chuo Kikuu cha Los Angeles ( UCLA) na Taasisi ya Utafiti ya Stanford ( SRI) walijiandaa kutumiana data kati yao. Lilikuwa ni jambo ambalo leo hii tunaliona la kawaida sana, lakini 1969 lilishangaza wengi. Mhandisi mmoja wa Stanford alichapa herufi 'L' na kumpigia simu mwenzake wa Los Angeles kama alipokea herufi hiyo, mwenzake alisema kuwa herufi hiyo ilimfikia. Baada ya hapo, kilichofuata ni historia, mtandao ulipokolewa rasmi na wanadamu.

Marekani ya 1969 ilikuwa ni nchi iliyokwisha tandaza mawasiliano ya simu nchi nzima na hivyo kuwa rahisi kwa mtandao wa internet kusambaa kuanzia pwani ya mashariki( Chicago) mpaka pwani ya magharibi ( california). Tofauti na Marekani, nchi nyingi za Bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara zimeingia karne ya 21 zikiwa hazina mawasiliano ya uhakika ya simu za mezani( Landline). Katika ile hali ya kupigana na ukweli halisia, baadhi ya nchi za kiafrika zinajikongoja na kuchukua hatua za kurekebisha mambo. Nchini Uganda, serikali ilichukua hatua ya kusambaza teknologia ya mawasiliano ya mtandao nchi nzima hasa vijijini ambapo kampuni za za binafsi zilishindwa kuwekeza huko kutokana na kushindwa kung'amua faida. East African ( gazeti la kila wiki la ukanda wa Afrika mashariki) linaripoti kwamba Uganda Communication Council ( UCC) ilichukua jukumu la kufikisha teknologia ya mawasiliano ya mtandao kwenye wilaya na vijiji katika juhudi za kujaza uwazi wa 'digital divide' kati ya mijini na vijijini. Bado mkakati huo umeshindwa kwani council iliyaachia uongozi wa wilaya hizo gharama za kuendesha miradi hiyo bila serikali kuwekeza kwa kina. Vile vile viongozi wa wilaya wamekuwa wakilalamika kwamba tatizo la umeme vijijini limekuwa kikwazo cha utekelezaji wa zoezi hilo.



Ili internet iweze kufanya kazi umeme ni suala lingine linalotatiza nchi nyingi za kiafrika. Tuchukulie mfano, Tanzania, ambayo hivi karibuni imekuwa katika tatizo la mgao wa umeme. Hii ina maana kwamba computer zetu haziwezi kufanya kazi panapokosekana umeme. Ingawa wadau wamekuwa wakitandaza generators kama suluhisho mbadala, bado umeme ni tatizo linatuweka waafrika nje ya ngoma ya kizungu ya mtandao. Hata hapo Tanzania inapokuwa haina mgao wa umeme, bado usambazaji wa ugavi huu haujafika nchi nzima, ni asilimia 11% tu familia za Tanzania zina umeme ikilinganishwa na 100% ya Marekani.



Elimu je,? bado rasilimali watu yahitaji kupigwa msasa wa uhakika kama kweli tunataka kukumbatiwa na dunia ya mtandao. Elimu nzuri na ya kisasa ni chachu ya maendeleo ya teknologia na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Nina mdogo wangu aliyepo kidato cha tano ambaye hajawahi kuwasha computer. Vyombo vya habari vya Tanzania hivi karibuni vili ripoti kuwepo kwa mwanafunzi wa kidato cha tatu mkoani Arusha hasiyejua kusoma na kuandika. Ikumbukwe kwamba matumizi ya komputa hayawezekani bila kujua kusoma na kuandika!!


Miaka 40 iliyopita, miundombinu ya Marekani ilikuwa tofauti sana na miundombinu ya Tanzania. Amerika ina ukubwa wa 9,161,923 sq km, ambayo ni karibu ya mara kumi ya Tanzania yenye ukubwa wa 945087 sq km, lakini Amerika ya 1969 ilikuwa imeunganishwa na miundombinu yenye uhakika, yaani barabara, miundombinu hii ni muhimu sana katika ufanisi wa uchezaji wa ngoma ya mtandao.

Hii ina maana kwamba Amerika ya 1969 ilikuwa imejiandaa kupokea teknologia ya mtandao kwa mapana kabisa. Leo hii hapa Tanzania msafiri anayetoka Dar es Salaam kwa usafiri wa basi kuelekea mkoani Kagera anapoteza masaa 30, wakati usafiri wa ndege kutoka hapa kuelekea London ni masaa 9. Inachukua masaa matatu kutoka Tegeta ( nje kidogo ya Dar Es Salaam) kuelekea kati kati ya mji, umbali wa kilomita 28, wakati ni masaa 4 kuendesha gari kutoka Reading town ( Uingereza) kuelekea Leeds, umbali wa kilomita 265!!

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, ' wakati wenzetu wanakwenda mwezini, siye bado hatujafika kijijini'.

Faida mojawapo ya internet ni kuwezesha manunuzi ya bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. E-commerce ni mbinu ya kibiashara inayotamba katika karne hii ya 21 na huko Ulaya na Amerika vitu vinanunuliwa kupitia tovuti maarufu kama vile ebay, amazon, Japanesevehicles, n.k.Matumizi ya e-commerce kwa wakazi wengi wa Afrika itaendelea kuwa ndoto kwani barabara zetu ni mbovu sana hivyo uharaka wa internet unaonekana hauna maana.E-commerce imeharakisha biashara ya wenzetu waliondelea kwa kiwango kikubwa hivyo kuwaongezea faida. Barabara za Afrika, ni mbovu zilizo na muonekano wa maandaki na hivyo kuchelewesha usafirishaji wa bidhaa. Nchini Uganda kuna utani kwamba ukimuona dereva anaendesha katika mstari ulionyooka basi huyo ni mlevi.

Hata hivyo baadhi ya nchi za kiafrika zinajitaidi kuwafikishia wananchi wake walioko vijijini teknologia ya mawasiliano kwa kutumia njia nyingine mbadala katika ile hali ya kuyashinda mapungufu ya miundombinu finyu. Hivi karibuni Rwanda imeanzisha utaratatibu wa e-bus ambapo mabasi mawili yenye vifaa vya kisasa vya mtandao yamekuwa yakizunguka sehemu za vijijini. Mabasi hayo yana laptops zilizounganishwa na mtandao, printers, na scanners, na vile vile yana generators hivyo kufanikiwa kufanya kazi hata katika yale maeneo yasiyo na nishati ya umeme. Watunga sera wa kinywarwanda wanaamini kwamba e-bus itawezesha wakulima wadogo wadogo kujua bei za mazao, kujifunza kilimo cha kisasa, kutambua hali ya hewa katika muda muafaka, na hivyo kuunganishwa kiukweli na soko la Dunia. Inaaminika vile vile kwamba wanafunzi waliopo vijijini wataweza kujifunza kwa vitendo teknologia hii muhimu ya mawasiliano hivyo kufanikiwa kuziba pengo la 'digital divide' kati ya wakazi wa vijijini na mijini.

Kwa ujumla, ingawa nchi za kiafrika zimekuwa zikipanga mipango ya zima moto! na kujaribu kukimbia na kasi ya mawasiliano, bado inatubidi tuwekeze kwa mapana katika miundombinu ya msingi, yaani barabara, simu, umeme, na elimu ya kisasa. Serikali za kiafrika haziwezi kuwaachia wawekezaji binafsi jukumu lake muhimu la kuendesha nchi zao, hasa katika suala la uwezekaji kwa wananchi wake. Mwalimu nyerere aliwahi kusema kwamba hana matatizo na sera za kibepari, bali akasema anataka manahodha wa kibepari, siyo mabepari uchwara. Hivi karibuni kumekuwa na kelele nyingi za mitandao inayokwenda kwa kasi sana, mitandao ambayo zimefaidisha wakazi wachache wateule ( elites) wa mijini badala ya kusambaa nchi nzima.

Mungu ibariki Afrika.

No comments:

Post a Comment