Sunday, November 8, 2009

Tambaza Sekondari


Moja wapo ya darasa la shule kongwe iliyotamba sana miaka ya 1970 80' na mwanzoni ya 90'. Ni kielelezo wazi cha jinsi ambavyo serikali imekubaliana na sera za kigaidi za magharibi, structural adjustment programmes. Baada ya nchi za kiafrika kuzidiwa na madeni ya nchi za magharibi, na baada ya wapambe wetu, wa mashariki ( USSR) kuishiwa nguvu ya kifedha, sasa tulilazimishwa kuachana na uwekezaji katika sekta muhimu za maendeleo, elimu ikiwemo.
Nani anajali? Tambaza ya leo imekuwa ya walalahoi, siye twapeleka watoto wetu shule za binafsi. Iko wapi sera ya elimu ya kitaifa?
Miaka hiyo sie tulipokuwa tunamaliza shule ya msingi, Tambaza sekondari ilikuwa ni ndoto ya kila mtoto aliyekuwa LY ( last year). Tambaza, Azania, Forodhani, jangwani, na Zanaki zilikuwa ni shule zilizokuwa ni uchaguzi wa wanafunzi wengi. Hatukuwa na utitiri wa shule za 'academies' kama tulizonazo sasa. Kwa siye tuliyefeli ( hatukuchaguliwa) ilituuma sana kwa kutochaguliwa kwenda Tambaza au Azania. Miaka hii mwanangu anapochaguliwa kwenda Tambaza nakataa kumpeleka huko, na kumtafutia shule za binafsi kama vile Alfa High School, St Mary's, nk. Kinachasikitisha hata wale 'vigogo' hawawapeleki watoto wao Tambaza.
Inapofikia mahala hatuna sera iliyonyooka ya elimu, kila mtu anachukua chake mapema. Tunapiga kelele kila kuhusu vita ya ufisadi, tunasahau kwamba tunajaribu kutibia ugonjwa badala ya kutibia chanzo cha ugonjwa. Hakuna mwafrika hasiyependa maisha mazuri kwa watoto wake, tunapenda watoto wasome pazuri, wale chakula kizuri, waishi nyumba nzuri, na wawe na uhakika wa maisha ya baadaye. Ni pale serikali inaposhindwa kutoa maisha bora ndipo hapo rushwa ndogo ndogo ( kwa wale walio chini) na kubwa kubwa ( kwa wale viongozi) inaposhamiri.

No comments:

Post a Comment