Sunday, January 10, 2010

NI NCHI YA WATU WADOGO


Hiyo ni jina la wimbo wa mwanamuziki Erick Wainaina kutoka Kenya aliyotoa kibao hicho akisanifu hali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya nchi ya Kenya.

Siyo Kenya, tu bali sehemu kubwa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, hali ni ile ile. Hapa Tanzania tunaitwa wananchi; na hapo ndipo ninapoanza kutia mashaka ya mwenendo wetu waafrika. 'wananchi' inatokana na neno, 'wana' yaani watoto. Na 'mtoto' sharti apewe mahitaji yake na 'Baba' mpaka afike ule umri wa
kujitegemea.

Kwa bahati mbaya sana, dola za kiafrika kwa manufaa yao binafsi wangependa wataliwa waendelee kuwa wananchi mpaka Yesu atakaporudi. Hii inapelekea uundwaji wa mataifa ya ombaomba na hata ubunifu kidogo alionao mwanadamu unaondolewa kutokana na dhana ya utegemezi unaopaliliwa na viongozi wetu.

Iko wapi Siasa ya ujamaa na kujitegemea? Ingawa wengi watahoji na kujiuliza kwani siasa ya ujamaa na kujitegemea mbona ilidumu kwa miongo takribani mitatu na hatukuendelea? Ninachoweza kujibu ni kwamba aghalabu siasa hiyo iliweka msingi wa kuendelea na ilikuwa ni kazi ya dola kujenga nyumba imara. Abraham Lincoln aliyekuwa Rais wa Marekani aliwahi kuwauliza wamerekani. 'Jiulize utaifanyia nini Marekani, na siyo Marekani itakufanyia nini'. Enzi ya Mwalimu watanzania tulipelekwa katika mwelekeo wa kujitegemea zaidi ya kutegemea. Mtoto wa shule ya msingi bila ya kuwa na tabaka lolote alitegemewa kwenda shule na ufagio wa chelewa kwa wale tuliosoma mjini na kwenda na jembe kwa wale waliosoma vijijini. Shule ya sekondari ilimjenga mwanafunzi kuwajibika mashambani na hata pale alipomaliza kidato cha sita tulitegemewa kujiunga na jeshi la kujenga Taifa. Hii yote ilikuwa ni katika hali ya kujenga misingi ya kujiamini na kuamsha chachu za kukomaa, ubunifu na kudumisha mapenzi kwa nchi. Mtanzania alijengwa na kuandaliwa kuwa mkulima au mfanyakazi na siyo ombaomba.

OMBA OMBA sasa inaanaanza kuwa ni sehemu ya maisha, yaani ustaarabu wetu, jambo linalonikera kweli kweli. Hata ubunifu na uvumilivu kidogo kama binadamu unatushinda. Hainiingii akilini pale ambapo mtu ananijia na mali mathalani nguo inayochuuzwa na ndugu yake na kuniomba ninunue eti ili nimuunge mkono huyo ndugu yake. Wenyewe tunasema 'muungishe' ndugu yangu. Sasa najiuliza, je nanunua shati kwa sababu ninalihitaji ( need) au kwa sababu ili nikusaidie kuyamudu maisha ya mjini? Hainingii akilini pale ninapoegesha gari langu likiwa safi kabisa na anatoka kijana akiwa na ndoo ya maji akiomba alioshe gari na mwisho wake nimpatie pesa. Ninamwambia kuwa liache hili gari langu ni safi, huyo kijana mwenye nguvu zake za kuendeleza sera ya kilimo kwanza mashambani ananijibu, basi naomba nilioshe unisaidie maji ya kunywa, yaani pesa kidogo. Sasa kijana huyu anauza huduma yake ya kuosha gari au anaomba msaada wa pesa? Heshima ya mtanzania inashuka sana pale mfanyakazi mwenzako ambaye kwa bahati mbaya sana ana mshahara mdogo kukupita wewe anapokuomba, 'Bosi nifanyie 500/= sijala ndugu yako'. Nani atakataa nikisema kuwa nitakapompatia hiyo 500/= ninamdumaza na kudumuza 'utoto wake, i.e mwananchi. Na miye ninayetoa hiyo pesa ninakuwa 'mwenyenchi'.

JE TUTAFIKA?

No comments:

Post a Comment