Sunday, October 25, 2009

KURA YA NINI? SERIKALI NI MFU!!!

Jumapili iliyopita watanzania kote nchini walitarajiwa kupiga kura kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa katika ile hali ya kutimiza haki zetu za kimsingi za kikatiba, yaani kuchaguliwa ama kuchagua viongozi tunaotarajia watatuletea maendeleo katika vitongoji vyetu.

Kwa mujibu wa Waziri wa nchi anayeshughulikia serikali za mitaa, Mheshimiwa Celina Kombani namba ya waliojiandikisha kupiga kura nchi nzima ni sawa na 53% ya watu millioni 16.1 ambao serikali ilikadiria wangejiandikisha kupiga kura.

Uchaguzi umeisha salama na umefanyika katika vituo 66,136 vilivyoko katika vijiji 11,197 na mitaa 2,606 katika halmashauri 132 nchini, ambapo viongozi 279,925 wamechaguliwa katika ngazi ya vijiji na vitongoji, na 15,636 katika ngazi ya mitaa.

Chama Cha Mapinduzi, CCM kimeibuka na ushindi mkubwa ambapo kwa mkoa wa Dar Es Salaam wajumbe 34 walipita bila kupingwa ambapo mkoani mbeya wajumbe 4000 wa CCM kati ya 5,592 vile vile nao wamepita bila kupingwa.

Licha ya haya yote mimi mkazi wa Tegeta, Dar Es Salaam sikupiga kura, wala sikujua sehemu iliyokuwepo kituo cha kupigia kura.



Sababu ni nyingi lakini zaidi ni ule ukosefu wa mwamko wa kisiasa siyo tu kwa mimi kama mtanzania bali pia kwa watanzania wenzangu ambao niliwaona wakiendelea na maisha yao ya kila siku pale mtaani kwangu. Kuna waliokuwa kwenye maduka yao ingawa hii ilikuwa ni siku ya kumwabudu Mungu kwa walio wakristu, kuna niliowaona wakibeba ndoo za maji kichwani wakiangaika kutafuta maji, kwa wale wakulima niliwaona wakimwagilia michicha yao,na waangaikaji wengine niliwaona wakisukuma mikokoteni. Jirani yangu aliendelea kusimamia mafundi wanaomjengea nyumba yake. Kwa kifupi wengi hatukustuka na uchaguzi huu.



Waziri Kombani alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari siku mbili kabla ya uchaguzi alikiri kuwepo na idadi ndogo ya watanzania waliojindikisha kupiga kura. Alisema kuwa wengi waliojindikisha ni wananchi wa vijijini ambapo 30% walijiandikisha ambapo maeneo ya mijini namba ilikuwa ya chini zaidi. Akaainisha kuwa sababu mojawapo ya idadi ndogo ya wapiga kura maeneo ya mijini ni uelewa mdogo ( ignorance) wa watu wanaofikiri kuwa uchaguzi hauna manufaa kwao. Vile vile Radio ya binafsi yenye makao yake makuu jijini Dar Es Salaam, Clouds Fm ilitoa takwimu ya watu 500,000 waliopiga kura katika jiji la Dar Es Salaam kati ya wakazi wa jijini.

Lakini mie naona ni ukweli kuwa uchaguzi hauna maana hasa kwa mtu wa kawaida kwani hakuna kitu anachoweza kujivunia kuwa ni kazi ya viongozi aliyewachagua katika uchaguzi uliopita. Wananchi hawategemei barabara zijengwe na viongozi wao hapa mitaani mwetu, wala hatutegemei kujengewa kituo cha polisi karibu na makazi yetu bila kuweka nguvu zetu wenyewe, wala hatuwaambii wajumbe wa mitaa yetu wakusanye takataka kwa niaba yetu. La hasha! wananchi kwenye vitongoji wanakosa viongozi wa kuwahamasisha, wanakosa viongozi wa kuwaongoza, viongozi watakaoonyesha njia ya kuelekea kwenye maendeleo ya kweli. Tunaliliona kwenye mitaa na vitongoji vyetu ni viongozi bubu, wasiotoa maelezo yenye tija; na tunapofika hapo nchi inakuwa inaingia kwenye mashaka sana. Viongozi wanadharaurika na kila mtu anachukua uamuzi kwendana na mazingira yake.

Katika nchi yenye mtazamo makini, wananchi wanatarajiwa kuilinda na kuitetea katiba yao, na upigaji kura ni njia sahihi ya kutimiza adhima hii. Mwalimu Nyerere ( Nyerere 1995) aliwahi kuandika kuwa wakati wote wananchi wanaweza kuitetea katiba kama wanajua wakati wote wawakilishi wao wanafanya nini kwa niaba yao. Kama hawaambiwi ukweli kinachotokea ndani ya nchi yao wananchi hawa watawezaje kuitetea katiba?



Hapa kwangu Tegeta na sehemu nyingi za Dar Es Salaam ni kila mtu na lwake! mtu anachoweza kufanya yeye kama mtu binafsi anakifanya bila kushirikishwa au kuhamasishwa na kiongozi wake wa mtaa. Ninapoamua kujenga ukuta kwenye nyumba yangu hii inamaana ninajiwekea kizuizi na jumuiya inayonizunguka. Ninapoweka simtank la maji ya ziada ina maana sitarajii na wala sitalalamika pale DAWASCO watakaposhindwa kunipatia huduma ya maji. Ninaponunua LandCruiser, na kulipitisha kwenye barabara mbovu iliyojaa mashimo mfano wa mahandaki ina maana sitarajii mwenyekiti wa serikali za mitaa kuitisha mkutano wa wananchi kujadili njia mbadala ya kuweka vifusi kwenye barabara za vitongoji vyetu. Wazungu wanasema 'Its a private solution for the public problem'

Fanon(1963, p. 119) analielezea tabaka la wasomi ambalo baadhi yao linajiingiza kwenye siasa kama ifuatavyo;

Inaonekana kwamba tabaka la wasomi halijajiandaa, wala halina uhusiano au ukaribu wa kimatendo ( practical) na umati wa watu, ule uvivu wa hili tabaka la wasomi, na uwoga wao katika muda muafaka wanapotarijiwa kutimiza majukumu yao ya kimapigano huleta hasara kubwa kwa jamii.

Hata baada ya miaka zaidi ya 40 tangia tupate uhuru, mapigano ya sasa siyo yale ya kumuondoa mkoloni, bali vita ya sasa ni kuuondoa ukoloni mamboleo unaokuja kwa sura ya utandawazi ( globarization). Lakini kama vile anavyoanisha Issa Shivji (2007) viongozi wanaoshika madaraka nchini kwetu wanaimba wimbo wa ukoloni mamboleo badala ya kuupinga wakiwa bega kwa bega na wapiga kura wao.

Kiongozi wa mtaa ninaemtaka mimi ni yule atakayetambua kuwa mipango ya ukoloni mamboleo ndiyo iliyosababisha bei zetu za mazao vijijini kushuka bei mno hivyo kulileta kundi kubwa la vijana mjini. Ni kiongozi atakayekuja na mipango endelevu ya kulipa ajira jeshi hili la vijana ndio atakayenifanya nipige kura ya kumchagua.

Kiongozi ninayemtaka mimi ni yule atakayetambua kuwa elimu inayotolewa na serikali ni afifu mno hivyo kuja na mipango inayowashirikisha wananchi wa mtaani ambao wote wanapenda watoto wao kusoma shule katika mipango ya kujenga maktaba, au shule ya kisasa.

Serikali yetu imekufa! a stateless society!!! No police, no healthcare, no fire brigade, no proper public schooling, no adequate water supply, infrequent power supply, and above all no effective leadership.



Mungu Ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment