Friday, October 16, 2009

NI UMASKINI WA MAWAZO SIYO HALISIA


Leo Dunia inatubeza siye wa nchi 'maskini' kwamba ni sikukuhuu yetu! Inaitwa siku ya umaskini Duniani. Kiukweli siye wa nchi za ulimwengu wa tatu siyo maskini bali umaskini wetu ni wa mawazo tu. Viazi vitamu vinakubaliana na hali ya joto hivyo kwa akili ya kawaida vingetakuwa viwe vinatawala kwenye meza zetu kama sehemu ya kifungua kinywa. Ila kwa sababu tunapenda sana kuiga chakula wanachokula wale waliotutawala basi tunaona vyetu ni vya kishenzi. Watawala walipokuja na mkate na siagi tukaona viazi vyetu havina mpango. Wahaya wanaita viazi vikuu, ebitakuli, maana yake ni Hivi weka pembeni. Kuna stori kwamba muhaya mmoja alipowekewa vyakula vingi mezani alichagua vyakula vingine na kuachana na viazi vikuu.

Leo hii husipokula mkate na siagi unaonekana umeishiwa na watoto wa mjini wanasema 'umefulia'. Kinachosikitisha zaidi ni kwamba baadhi ya vitafunwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi hivyo tunapoteza pesa zetu za kigeni. Weetabix inatoka Uingereza na siku za baadaye itachukua nafasi ya mkate.

Msomi ninayependa kusoma kazi zake Ali Mazrui katika kitabu kinachoitwa 'The Africans' aliandika, ninamnukuu katika lugha ya kiswahili.


Katika kipindi cha kizazi kimoja kilichopita tumeshuhudia kasi kubwa ya waafrika kuiga mila za kigeni na ufuatiliaje wa maisha ya ughaibuni. Kama wayahudi waliokimbilia nje ya nchi yao wangediriki kubadilisha ustaarabu wao kwa haraka kama waafrika wanavyofanya ndani ya nchi zao, maajabu ya utambulisho wa kiyahudi yasingedumu katika millennia mbili au tatu walizokaa mbali na nchi yao. Hata sasa waafrika wengi wanaonekana kubadilika kwa kasi kubwa kiutamaduni katika kizazi kimoja zaidi ya wayahudi walivyobadilika ndani ya miaka 1000 nje ya nchi yao.

Mchele unaliwa dunia nzima, lakini muhogo ni wakwetu, wakwetu asilia. Zao la muhogo linaweza kuchemshwa, kuchomwa, kubanikwa, kukaangwa, na kupikwa kama chakula cha mchana. Vile vile muhogo unaweza kukobolewa na kupatikana unga mtamu wa ugali, tunaweza vile vile kunywa uji wa muhogo na hivyo kuachana na weetabix. Majani ya muhogo maarufu kama kisamvu ni chakula kinachodharauriwa na watanzania hasa wa mjini eti ni mlo wa kimasikini.

Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Pinda alituasa watanzania tuache kuwa na kasumba ya kupenda mchele na unga na kuacha mazao yanaostahimili ukame kama mihogo. Tumekariri kuwa mchele na unga kuwa ni vyakula vikuu na hata wakati mwingine ukame unavyokamata tunaagiza nafaka hizi kutoka nje ya nchi na kutumia pesa chache za kigeni tulizonazo. Inasikitisha tunapoona wachaga hawali mihogo kwa ujinga tu kwamba zao hilo ni sumu. Ni ujinga vile vile kuwaona wahaya wanakufa njaa eti kwa kuwa ndizi zimeingiwa na wadudu. Inauma kuona wahaya wanakosa pesa ya kujikimu eti kwa kuwa kahawa imekosa soko duniani. Kwanini wahaya wasilime mihogo na kuwauzia wakazi wa mijini wanaopoteza pesa kuagiza weetabix?

Waafrika tumekuwa watu wakusaidiwa kiuchumi na hata kimawazo, tuchukulie mfano wa tajiri mkubwa mmiliki wa Microsoft, Bill Gates aliyezindua hivi karibuni mpango wake wa kilimo endelevu kinachozingatia mazao ya nyumbani ili kunusuru Bara la Afrika na janga la njaa. Mpango huo utakaogharimu dollar million 120 unalenga kutuelimisha waafrika umuhimu wa kupanda mazao kama viazi vitamu ambavyo vinasifika kutokomeza mapungufu ya Vitamin C hasa kwa watoto.

Mawazo endelevu na yenye nuru ya Gates yanaungwa mkono na Dr Hartmann, Mkurugenzi wa shirika la kitafiti linalotafuta ufumbuzi wa njaa na umaskini wa kiafrika liitwalo IITA. Kwenye mahojiano na The Guardian, 17 of October, mtafiti huyu anatoa angalizo kwamba walaji wa kiafrika inabidi wasaidiwe kujifunza kubadilisha jinsi wanavyokula ili wasiwe wanategemea mazao machache. Anaanisha kwamba nchi zilizoadhirika zaidi na njaa ni zile zinazotegemea mchele, mahindi na ngano mazao ambayo ni maarufu katika soko la dunia. Wakati mazao hayo yamekuwa yakipanda bei siku za hivi karibuni, bei za mazao kama mihogo na viazi vikuu vimekua vikiwa na bei hisiyoteteleka.

Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa septemba 29 na Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na utafiti wa sera za chakula IFPRI yenye makao yake Washington, Marekani inahasa kwamba ifikapo 2050, Afrika kusini mwa jangwa la Sahara itapungukiwa na mavuno ya mchele kwa 14%, ngano 22% na mahindi 5%. Mapungufu haya yatakayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa yatazidisha hali ya utapiamlo hasa kwa watoto.

No comments:

Post a Comment